TAARIFA
KWA UMMA
KUHUSU
VYAMA NA WAGOMBEA KUZINGATIA MAADILI YA UCHAGUZI WA RAIS, WABUNGE NA MADIWANI
YA
MWAKA
2015
Kama mnavyofahamu Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Rais,
Wabunge na Madiwani zimeanza tangu tarehe 22 Agosti, 2015 na zinaendelea hadi tarehe
24 Oktoba, 2015.
Ni jambo linaloeleweka kwamba mchakato wa Kampeni
na wa Upigaji Kura unatawaliwa au kuongozwa na Sheria, Katiba na Maadili ya
Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015.
Katika kipindi hiki tangu Kampeni zianze, nafurahi
kusema kwa niaba ya Tume kuwa kwa ujumla, Kampeni zimeenda vizuri. Karibu mikutano yote imefanyika katika hali
ya utulivu na amani. Hatujapata taarifa
ya mkutano wa Kampeni ambao umevurugwa kwa fujo zozote. Kwa hilo napongeza Vyama vyote vya Siasa.
Hata hivyo, kutokana na mikutano hiyo nchini ya
Kampeni, ngazi ya Urais, Ubunge na Udiwani yamejitokeza mambo ambayo ni kinyume
kabisa na Mwongozo wa Maadili ya Uchaguzi wa Rais Wabunge na Madiwani wa mwaka
2015 uliotiwa saini na Vyama vyote vya Siasa tarehe 27 Julai, 2015.
Yafuatayo ni baadhi ya mambo ambayo yamejitokeza
katika Kampeni hizo:-
(i)
Kutozingatia
muda wa kumaliza Mikutano ya Kampeni
Kuna baadhi ya Vyama ambavyo katika mikutano yao
vimekiuka Kipengele hiki kwa kufanya mikutano zaidi ya saa 12.00 jioni. Kuendelea kufanya Mkutano wa Kampeni zaidi ya
muda huo ni ukiukwaji wa Kipengele cha
2.1 (c) cha Maadili ya Uchaguzi wa
Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015 kinafafanua kuwa Mikutano yote ya Kampeni
itafanyika kuanzia saa 2.00 asubuhi hadi saa 12.00 jioni.
(ii)
Kubandika
mabango ya Kampeni, matangazo au Mchoro wowote kwenye maeneo yasiyoruhusiwa au
bila idhini ya wahusika
Baadhi ya Vyama vimeanza kubandika mabango, michoro
na picha za Wagombea wao katika majengo au vyombo vya usafiri vya watu binafsi
au Taasisi mbalimbali bila idhini ya wamiliki husika.
Napenda kuwakumbusha kuwa, kwa mujibu wa Kipengele cha 2.2. (g) cha Maadili ya
Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015, hairuhusiwi kufanya hayo
bila idhini ya wamiliki husika.
(iii) Kuchafua, kubandua au kuharibu
matangazo au picha za Kampeni za Vyama vingine
Tume imeanza kupokea malalamiko kutoka baadhi ya
Vyama kuwa, mabango au picha za Kampeni za Vyama vyao yanabanduliwa au
kuchafuliwa na wafuasi wa Vyama vingine.
Ni vema Vyama vya Siasa na Wagombea wakumbuke kuwa Kipengele cha 2.2 (f) cha Maadili ya
Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015, kinapiga marufuku Chama
kingine kuchafua, kubandua au kuharibu matangazo au picha za Kampeni za Vyama
vingine.
(iv) Matumizi ya lugha zisizo za staha
Tume imepokea malalamiko kuwa, katika Mikutano
mbalimbali ya Kampeni katika ngazi zote, kumeanza kujitokeza baadhi ya viongozi
wa Vyama, Wagombea au wafuasi wao kutumia lugha zisizo za staha wakati wa Mikutano
ya Kampeni katika ngazi mbalimbali.
Lugha zisizo za staha zinajumuisha matusi, kejeli,
kashfa n.k. Kipengele cha 2.2 (b) cha Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na
Madiwani ya mwaka 2015, kinakataza Viongozi wa Vyama vya Siasa na Wagombea wao
kutumia lugha zisizo za staha katika harakati zote za Kampeni hadi upigaji
Kura.
Wajibu
wa Vyama vya Siasa na Wagombea
Viongozi wa Vyama vya Siasa na Wagombea wana wajibu
wa Kisheria wa kuyaheshimu, kuyasimamia na kuyatekeleza Maadili hayo kwa mujibu
wa Kipengele cha 2.1. (b) cha Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani
ya mwaka 2015. Viongozi wa Vyama vya Siasa na Wagombea wana jukumu la kuwaelimisha,
kuwahamasisha na kuwasisitiza wanachama wao kutekeleza Sheria ya Uchaguzi
(ikumbukwe kuwa Maadili ya Uchaguzi yametungwa chini ya Kifungu cha 124A cha
Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343)
Adhabu za
ukiukwaji wa Maadili ya Uchaguzi
Napenda kuwakumbusha Vyama vya Siasa na Wagombea
kuwa, ukiukwaji wa aina yoyote wa Maadili unaweza kusababisha Chama au mgombea
kupewa adhabu kama zilivyoainishwa katika Kipengele
cha 5.10 (a-f). Adhabu hizo ni pamoja na:
1.
Chama au Mgombea aliyekiuka
maadili kuelekezwa kuomba msamaha hadharani.
2.
Kupewa onyo au karipio.
3.
Kumtangaza kupitia vyombo
mbalimbali vya habari na taarifa kwa Umma mgombea au Chama kilichokiuka
Maadili.
4.
Chama au Mgombea kusimamishwa
kuendelea kufanya Kampeni.
5.
Chama au Mgombea kuzuiliwa kutumia
vyombo vya habari.
6.
Chama au Mgombea kulipa faini
kuanzia kiwango cha 100,000/- 500,000/- na 1,000,000/- kutegemea ngazi ya
Kamati husika.
Katika
kipindi hiki cha Kampeni, Chama au Mgombea akipewa mojawapo ya adhabu hiyo
kunaweza kuathiri Kampeni zake za kuelekea Uchaguzi wa Rais, Wabunge au
Madiwani.
Hitimisho.
Napenda
kunukuu Kipengele cha 1.4 cha
Maadili ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015 ili kila
Chama kione umuhimu wa kuwahimiza wagombea na wanachama wao kuzingatia Maadili
katika harakati zao za kujinadi. Nanukuu:
“[……] kila
mgombea atajaza Fomu Na. 10 kuthibitisha kuwa ataheshimu na kutekeleza Maadili
ya Uchaguzi. [….] Mgombea atakayekataa kusaini Maadili haya atakataliwa au
kuondolewa kushiriki katika Uchaguzi kama Mgombea.”
Maana yake ni kwamba kila Chama, Mgombea na
Wanachama kwa ujumla wana wajibu kuheshimu taratibu zote za Kampeni hadi kupiga
Kura.
Yote yaliyokatazwa katika Maadili yazingatiwe na
Vyama vyote. Kama nilivyosema hapo awali
Tume imepata malalamiko kuwa baadhi ya Vyama na Wagombea wamekiuka Maadili ama
kwa kuzidisha muda wa Kampeni, au kuchana na kuharibu mabango, au kutumia lugha
chafu isiyo na staha; Haya yote Tume inakemea kwa nguvu sana na kusihi
Vyama vyote na Wanachama wao wote kuheshimiana, waeleze sera zao bila
kukashifiana.
Lengo na matumaini ya Tume ni kuwa na Kampeni za
utulivu na hatimaye wananchi kuwa na hali ya utulivu na amani ili Uchaguzi
ufanyike kwa amani na utulivu. Kwenye
hali ya utulivu na amani wananchi wataweza kupiga Kura ya utulivu ili kuamua
viongozi wanaowataka. Hiyo ndiyo
Demokrasia.
Nimalizie kwa kuwakumbusha Vyama vyote kuzingatia
Maadili ya 2015. Tume isilazimishwe
kuchukua hatua za kutoaadhabu kwa Vyama na Wagombea. Busara itumike katika mikutano yote ya
Kampeni.
Inawezekana, wote tukidhamiria,
“Play your Part”.
Jaji (Mst.) Damian Z. Lubuva
MWENYEKITI
TUME YA TAIFA YA
UCHAGUZI
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni