USIUZE KADI YAKO

USIUZE KADI YAKO

Focusradiotz

Jumatatu, 12 Oktoba 2015

MKUTANO WA TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI NA VYAMA VYA SIASA UNAOFANYIKA KATIKA UKUMBI NEW AFRICA HOTEL TAREHE 12/10/2015


  HOTUBA YA UFUNGUZI YA MWENYEKITI WA TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI KATIKA MKUTANO WA TUME NA VIONGOZI  WA VYAMA VYA SIASA KATIKA UKUMBI WA NEW AFRICA HOTEL TAREHE 12/10/2015.


Viongozi wa Vyama vya Siasa,
Mheshimiwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa Ya Uchaguzi,
Waheshimiwa Makamishna wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi,
Mkurugenzi wa Uchaguzi,
Inspekta Jenerali wa Polisi,
Msajili wa Vyama vya Siasa,
Viongozi wa Serikali,
Watendaji wa Mradi wa Uimarishaji wa Demokrasia (DEP),
Watendaji wa Tume,
Waandishi wa Habari,
Mabibi na Mabwana.

Kwa niaba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, napenda kuchukua nafasi hii kuwakaribisheni wote katika Mkutano huu wa kujadiliana na kubadilishana mawazo kuhusu masuala mbalimbali  ya  Uchaguzi pia  kupeana taarifa kuhusu maandalizi ya Uchaguzi Mkuu utakaofanyika tarehe 25 Oktoba 2015.
Pamoja na kwamba mna majukumu mengi na ya muhimu mmetambua umuhimu wa mkutano wetu na mmekuja kuhudhuria mkutano huu kama ilivyotarajiwa. Tume imefarijika  sana kukutana nanyi siku ya leo na tunawashukuru kwa moyo mliyoonyesha katika mchakato huu wa maandalizi ya Uchaguzi na wa kututhamini na kuja kuhudhuria Mkutano wetu.

Viongozi wa Vyama vya Siasa,
Pamoja na changamoto mbalimbali mnazokabiliana nazo  katika kutekeleza majukumu yenu kisiasa  ni ukweli ulio dhahiri, kuwa Viongozi wa Vyama vya Siasa ni Wadau  muhimu wa  Uchaguzi ambapo  mkishirikiana kutekeleza majukumu yenu kwa ufasaha mtaleta mafanikio katika uendeshaji wa Uchaguzi.

Viongozi wa Vyama vya Siasa,
Vyama vya Siasa vina nafasi kubwa katika kuelimisha na kuhamasisha jamii, Tume inaamini kwamba ili Mpiga Kura aweze kufanya maamuzi sahihi ni muhimu kwake kupate Elimu sahihi. hivyo basi, Tume inatarajia kuona mkitumia majukwaa yenu vyema katika kuhamasishaji na kuelimishaji si tu wanachama wenu bali jamii nzima ya watanzania


Viongozi wa Vyama Vya Siasa
Kuelekea Uchaguzi Mkuu, Tume imeaandaa vituo vya kupigia kura 64,736, ambapo, Tanzania Bara ni Vituo 63, 156 na Zanzibar ni Vituo 1,580. Kila kituo kitakuwa na uwezo wa kuhudumia  Wapiga Kura  450 na wasiozidi 500. Hata hivyo Kituo kinapokuwa na  wapiga Kura zaidi ya 500 kinabidi kigawanywe ili viwe viwili yaani Kituo “A” na Kituo “B” na namba ya Wapiga Kura itakuwa nusu kwa nusu.  Wapiga Kura wanashauriwa kwenda katika vituo walivyojiandikishia kupiga kura siku nane (8)  kabla ya siku ya kupiga kura ili kuweza kujua Vituo vyao halisi vya kupigia kura.  Sambamba na hilo wananchi wataweza kupata taarifa zao zilizoko kwenye kanzidata (Database) kwa kutumia simu zao za kiganjani kupitia ujumbe mfupi wa maneno ‘sms’ bila wao kulazimika kufika vituoni, namba hiyo ni *152*00# na kufuata maelekezo. Au kupitia Tovuti ya Tume ambayo ni (www.nec.go.tz)



Viongozi wa Vyama Vya Siasa,
Tume imekuwa ikifuatilia kampeni za Vyama vyenu vya Siasa, hata hivyo Tume inasikitika kuona kuwa baadhi ya Vyama vya Siasa vimekuwa vikitumia majukwaa yao vibaya. Tume kwa namna ya pekee inawaomba katika kipindi hiki kifupi kilichobaki kutumia nafasi zenu majukwaani kuelezea sera za Vyama Vyenu ili kuweza kuwasaidia wananchi kufanya maamuzi sahihi baada ya kuwa na taarifa sahihi.

Viongozi wa Vyama Vya Siasa,
Tume imekuwa ikisikia katika vyombo vya Habari malalamiko mengi kuhusu uvunjifu wa maadili ya Uchaguzi katika kipindi hiki cha kampeni, naomba nitumie nafasi hii kuwaasa viongozi wa vyama vya siasa kupeleka malalamiko yenu  katika kamati za maadili na si kukimbilia katika Vyombo vya Habari kama ambavyo baadhi ya Vyama vya Siasa na Wagombea mmekuwa mkifanya.

Viongozi wa Vyama Vya Siasa
Tume inawaomba kuepuka kutoa taarifa na shutuma sisizo sahihi kuhusu Tume ya Taifa ya Uchaguzi badala yake mjikite katika kufikisha taarifa zilizo sahihi na zilizokusudiwa kwa Wafuasi wenu na wananchi wote kwa jumla, na pia kuwahamasisha wananchi kujitokeza kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa tarehe 25 Oktoba 2015.


Viongozi wa Vyama Vya Siasa,
Tume imejipanga kuhakikisha kila Mpiga kura  mwenye sifa za Kupiga Kura anapiga Kura yake pasipo kubughudhiwa. Ili kuhakikisha jambo hili linafanyika kwa ufanisi, Tume imetoa maelekezo kwa Makarani waongozaji vituoni kutoa upendeleo kwa watu wanaoishi na Ulemavu ili kuwasaidia waweze kupiga kura. Kwa wale wasioona Tume imeandaa kifaa maalumu cha nukta nundu ‘Tactile Ballot Folder’ ambayo itawasaidia katika upigaji kura kwa urahisi.

Viongozi wa Vyama Vya Siasa
Baadhi ya wagombea wamekuwa wakiwashawawishi Wapiga Kura wao kutoondoka katika Vituo vya Kupigia Kura baada ya kumaliza zoezi la Upigaji Kura, naomba nichukue nafasi hii kuwakumbusha kifungu cha 104 (1) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 kinasema nanukuu
Hakuna mtu atakayefanya Mkutano siku ya kupiga kura katika au ndani ya jengo lolote ambamo upigaji kura katika Uchaguzi unaendelea, au mahali popote ndani ya eneo la mita 200 ya jengo hilo, kuvaa au kuonyesha kadi ya picha yoyote, upendeleo au nembo nyingine inayoonyesha kuunga mkono mgombea Fulani katika Uchaguzi.“  mwisho wa kunukuu.
Aidha, kifungu cha 103 (1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292 kinasema, nanukuu:
“Hakuna mtu atakayeruhusiwa, katika jengo lolote ambalo upigaji kura katika Uchaguzi unaendelea, au njia yoyote inayotumiwa na umma ndani ya umbali wa mita tatu ya mlango wowote wa kuingilia katika jengo atavaa au kuonyesha au kuonyesha kadi, upendeo au nembo yoyote inayoashiria kumuunga mkono mgombea Fulani katika Uchaguzi” mwisho wa kunukuu.
Kifungu cha 5 cha Sheria ya Adhabu, Sura Na. 16 kinaeleza maana ya njia ya Umma. Nanukuu:
“Public way includes any highway, market place, square, street, bridge or other way which is lawfully used by the public”  Mwisho wa kunukuu.
Vifungu vya Sheria zote kwa pamoja havisemi wala kutoa fursa au nafasi kwa wananchi kukusanyika, zinapiga marufuku na kukataza uvaaji wa sare, au nembo au alama za Vyama vya Siasa siku ya kupiga kura kwa umbali kati ya mita 200 na 300.

Hivyo basi ieleweke kwamba umbali huo wa mita 200 mpaka 300 sio umbali unaowaruhusu watu kukusanyika kwa kisingizio cha kulinda kura.
Hivyo niwaase Wanasiasa kuzingatia Sheria na taratibu za uendeshaji wa Uchaguzi,  kuepuka lugha zozote za uchochezi zinazoweza kuleta uvunjifu wa amani na kuhatarisha maisha ya Watanzania.  Aidha uzoefu unaonyesha kwamba, katika Kampeni zinazoendelea, pale ambapo wafuasi wa Vyama tofauti wanapokutana uwezekano wa kutokea vurugu ni mkubwa na sehemu nyingine vurugu zimetokea na kusababisha maafa, majeruhi na uharibifu wa mali.

Hivyo, endapo kila chama kitaamua kuwaelekeza wafuasi wake kubaki kwenye Vituo vya Kupigia Kura uwezekano wa kutokea vurugu ambazo zinaweza kupelekea kuwatisha, kuwabughudhi, kuwatia hofu na kuwasumbua Wapiga Kura ni mkubwa hivyo kuhujumu zoezi la Upigaji Kura,
Zaidi ya hayo, maelekezo yaliyotolewa chini ya kifungu cha 126 na kifungu cha 63(2) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na kifungu cha 63(2) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura 292 na kifungu2.1 cha Maadili ya Uchaguzi ya mwaka 2015 yanasistiza kwamba kiongozi yeyote wa Chama cha Siasa anapaswa kuheshimu na kufuata maagizo yote ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Viongozi wa Vyama Vya Siasa
Kwa kumalizia ninapenda tena kuwashukuru wote kwa kuhudhuria Mkutano huu na Tume inaahidi kuyachukua mawazo yenu na kuyafanyia kazi yale yaliyomo ndani ya uwezo wetu ili kuweza kufanikisha Uchaguzi Mkuu wa mwaka  2015 kwa amani na utulivu.

Baada ya kusema hayo kwa niaba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, natamka kuwa Mkutano huu umefunguliwa rasmi.
Asanteni sana kwa kunisikiliza.


 JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI
MADA YA MAANDALIZI YA UCHAGUZI MKUU 2015
MKUTANO WA TUME NA VYAMA VYA SIASA UTAKAOFANYIKA KATIKA UKUMBI NEW AFRICA HOTEL TAREHE 12/10/2015.
12 Oktoba, 2015
page1image7304


1. UTANGULIZI:
Tume ya Taifa ya Uchaguzi inatarajia kufanya Uchaguzi Mkuu tarehe 25 Oktoba 2015 ukiwa ni Uchaguzi Mkuu wa tano (5) kufanyika tangu kuanzishwa tena kwa mfumo wa Vyama vingi vya Siasa mwaka 1992. Tangu kuundwa kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Januari, 1993, Tume imekuwa na mamlaka ya kusimamia na kuendesha Uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Madiwani kwa Tanzania Bara.



Katika chaguzi zilizopita, Tume ilifanikiwa kusimamia chaguzi hizo na kuelezwa na Waangalizi wa uchaguzi kuwa zilikuwa huru na haki isipokuwa kasoro ndogo ndogo zilizojitokeza. Kufanikiwa kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi katika kuendesha Chaguzi hizo kulitokana na ushirikiano na mchango mkubwa uliotolewa na Wadau mbalimbali vikiwemo Vyama vya Siasa, Serikali, Washirika wa Maendeleo, Vyombo vya Habari, Mashirika na Viongozi wa Dini na Asasi za Kiraia nk. Wadau wengi pamoja na mambo mengine kwa nafasi zao wamekuwa wakishiriki katika kuelimisha na kuhamasisha wananchi kujitokeza na kushiriki katika hatua mbali mbali za mchakato wa Uchaguzi.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi inaendelea na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2015. Katika kufanikisha Uchaguzi huo, Tume imekuwa ikikutana na Wadau mbalimbali wa Uchaguzi mkiwemo nyinyi Viongozi wa Vyama vya Siasa ili kupeana taarifa na kubadilishana mawazo kuhusu namna ya kufanikisha Uchaguzi huu. Tume ya Taifa ya Uchaguzi mara zote inatambua mchango wa Vyama vya Siasa katika kufanikisha chaguzi mbalimbali hapa nchini. Hii ni kutokana na weledi ambao mmekuwa mkionyesha katika kuelimisha na kuhamasisha wananchi kushiriki katika shughuli mbalimbali za kisiasa na kimaendeleo ikiwa ni pamoja na uchaguzi. Na hakika uhusiano wenu na Tume na uwajibikaji wenu umekuwa wa msaada mkubwa kwa Tume katika kufanikisha shughuli za Uchaguzi katika mazingira ya haki, sawa, na ya Amani.

Ni azma ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuhakikisha kwamba kila raia wa Tanzania mwenye sifa na aliyejiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura anapata fursa ya kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi huo, lakini pia kuhakikisha kuwa Uchaguzi huo unafanyika kwa uwazi na unakuwa huru na wa haki zaidi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zilizowekwa ili kujenga Demokrasia na kuimarisha Utawala Bora.

2. MAANDALIZI YA UCHAGUZI MKUU
2.1. Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura .
Tume imefanya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa kuandikisha Wapiga Kura upya uboreshaji huu ulihusisha:
1. Wapiga Kura waliokuwepo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura lililotumika mwaka 2010.
2. Wapiga kura wenye sifa ambao hawakuwa wameandikishwa hapo awali
3. Wapiga Kura wapya wenye sifa za kuwa Wapiga Kura na wale ambao watatimiza umri wa miaka 18 ifikapo siku ya Uchaguzi.
Katika Uandikishaji huu, Tume ilitumia teknolojia ya kisasa ya Biometric Voters Registration (BVR) na Wapiga Kura wote walipatiwa kadi mpya za kupigia kura aina ya “PVC” zenye alama za kiusalama.
Uandikishaji kwa mfumo wa BVR ulihusisha uchukuaji upya wa alama za kibaiolojia (Biometric features) ambazo ni picha, saini na alama za vidole vyote kumi (10) na kuzihifadhi kwa ajili ya utambuzi wa baadae. Mfumo huu umeiwezesha Tume kuandikisha Wapiga Kura wengi kwa muda mfupi na umewezesha kubaini wote waliojiandikisha zaidi ya mara moja.

2.2. Idadi ya Wapiga Kura
Tume ilikamilisha Uandikishaji wa Wapiga Kura kwa kutumia mfumo wa Biometric Voter Registration (BVR) tarehe 04 Agosti 2015, ambapo tulitoa taarifa za awali za watu walioandikishwa kuwa 23,782,558. Takwimu hii ilitokana na idadi ya taarifa za idadi ya walioandikishwa zilizopokelewa kutoka kwenye vituo vya kuandikishia Wapiga Kura.
Baada ya uhakiki na uchakataji (processing) wa taarifa za Wapiga Kura, Tume ilibaini kuwa:
1. Jumla ya taarifa za wananchi 181,452 walijiandikisha zaidi ya mara moja hadi mara nane kwa mtu mmoja.
2. Jumla ya taarifa za Wananchi 845,944 wamebainika ni wale ambao waandikishaji wa BVR Kits (BVR Kits Operator) ambao jumla yao walikuwa 74,502 walikuwa wanafanya mafunzo ya vitendo kabla ya kuanza uandikishaji wenyewe. Taarifa hizi zimefutwa katika kazidata ya Daftari.
3.Jumla ya taarifa 3,870 wamebainika kuwa waliandikishwa wakiwa sio raia wa Tanzania na hivyo, vitambulisho vyao vimerejeshwa na taarifa zao kufutwa kwenye kanzidata ya Daftari la Kudumu.
Hivyo, jumla ya taarifa za Wapiga kura 1,031,769 zimefutwa kutokana na sababu tajwa hapo juu.
Kwa maana hiyo, idadi halisi ya Wapiga Kura katika Daftari la Kudumu la Wapiga la Kura ni 22,751,292 waliandikishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na 503,193 waliandikishwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC)
2.3. Idadi ya Vituo vya Kupigia Kura
Kuelekea Uchaguzi Mkuu, Tume imeaandaa vituo vya kupigia kura 65,105, ambapo, Tanzania Bara ni Vituo 63, 525 na Zanzibar ni Vituo 1,580. Kila kituo kitakuwa na uwezo wa kuhudumia Wapiga Kura 450 na wasiozidi 500.
Hata hivyo, Kituo kinapokuwa na wapiga Kura zaidi ya 500 kitagawanywa katika vituo viwili kwa idadi ya idadi sawa kwa kila kituo. Wapiga Kura wanashauriwa kwenda katika vituo
5
walivyojiandikishia kupiga kura siku nane (8) kabla ya siku ya kupiga kura ili kuweza kujua Vituo vyao halisi vya kupigia kura.
Sambamba na hilo wananchi wataweza kupata taarifa zao zilizoko kwenye kanzidata (Database) kwa kutumia simu zao za kiganjani kupitia ujumbe mfupi wa maneno ‘sms’ bila wao kulazimika kufika vituoni, namba hiyo ni *152*00# na kufuata maelekezo. Au kupitia Tovuti ya Tume ambayo ni (www.nec.go.tz)

2.4. Changamoto wakati wa Uandikishaji Wapiga Kura.
Wakati wa zoezi la kuandikisha wapiga Kura, changamoto zifuatazo zilijitokeza:
  1. Watu kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura zaidi ya mara moja
  2. Ugumu wa uchukuaji wa alama za vidole kutoka kwa Wapiga Kura, tatizo lililosababishwa na kazi za kiuchumi wanazozifanya Wapiga kura.
  3. Printa kuhitaji kusafishwa mara nyingi zaidi kutokana na mazingira ya vumbi katika Vituo vya uandikishaji.
  4. Dahana potofu kuwa mfumo wa BVR ni mfumo utakaosaidia kuchakachua matokeo
Pamoja na changamoto hizo Tume imeweza kufanikisha zoezi la uandikishaji kwa muda mfupi kwa kutumia “BVR Kits” 8000, hii imepelekea Tume kupata pongezi kutoka Tume za Uchaguzi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).
page6image11216

2.5. Ugawaji wa Majimbo
Tume inao wajibu wa kuangalia upya Majimbo ya Uchaguzi angalau kila baada ya miaka kumi. Mara ya mwisho Tume ilifanya hivyo kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010. Mwaka 2015 Tume imegawa Majimbo mapya 25, ambapo TAMISEMI imeanzisha Kata mpya 622. Majimbo hayo na Kata hizo zitashiriki katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Jumla ya Majimbo 264 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Kata 3,957 za Tanzania Bara zitashiriki katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015.

2.6. Uteuzi wa Wagombea
Tarehe 21/08/2015 Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilifanya uteuzi wa Wagombea wa Kiti cha Rais na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ubunge, na Udiwani
2.7. Idadi ya Wagombea Kiti cha Rais
Jumla ya Wagombea 8 wa nafasi ya Kiti cha Rais waliteuliwa
kuwa Wagombea kati ya hao mwanamke ni 1 na wanaume 7. 2.8. Idadi ya Wagombea wa Ubunge

Jumla Wagombea 1,218 wa nafasi ya Ubunge waliteuliwa, Kati ya hao Wanaume ni 985 na wanawake ni 233.

2.9. Idadi ya Wagombea wa Udiwani
Jumla ya Wagombea 10,879 waliteuliwa kuwania nafasi za
Udiwani kati ya hao wanaume 10,191 na wanawake 679. Mchoro 1: Wagombea Ubunge
Mchoro 2: Wagombea Udiwani


2.10.Rufaa za Wagombea
Baada ya zoezi la Uteuzi kukamilika Tume ilipokea Rufaa za aina mbili.
Aina ya kwanza ni rufaa ambazo waliongeliwa na Wasimamizi wa Uchaguzi kugombea nafasi za Ubunge au Udiwani.
Aina ya Pili, ni rufaa ambazo wagombea wanakata rufaa kupinga maamuzi ya Msimamizi wa Uchaguzi kutupilia mbali rufaa zao dhidi ya wagombea wa nafasi ya Ubunge au Udiwani.

Kwa mujibu wa kifungu cha 40 (6) cha Sheria ya Uchaguzi wa Taifa Na. 1 ya mwaka 1985 sura ya 343 na kifungu cha 44 (5) cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali ya Mitaa Na. 4 ya mwaka 1979 sura ya 292 vinatoa haki kwa mgombea ambaye hakuridhika na uamuzi wa Msimamizi wa Uchaguzi kukataa au kukubali pingamizi lililotolewa.
2.11.Rufaa za Wagombea Ubunge

Tume ilipokea jumla ya rufaa 56 za Wagombe Ubunge zilipokelewa na kuamuliwa. Aidha, jumla ya Wagombea wa Ubunge 14 waliokuwa wameenguliwa kugombea Nafasi ya Ubunge walirejeshwa kwenye kinyanganyiro hicho baada ya kukata rufaa, wagombea 2 wameendelea kuenguliwa baada ya rufani zao kukataliwa na jumla ya rufaa na Rufaa 40 Tume ilikubaliana na maamuzi ya Wasimamizi wa Uchaguzi.

2.12.Rufaa za Udiwani
Tume ilipokea jumla ya rufaa 223 za Wagombea Udiwani kupinga uamuzi wa Wasimamizi wa Uchaguzi katika Kata mbalimbali. Tume imepitia na kufanya uamuzi wa rufaa 218. Ambapo Wagombea wa Udiwani 50 waliokuwa wameenguliwa kugombea Nafasi ya hiyo walirejeshwa kwenye kinyanganyiro hicho baada ya kukata rufaa, wagombea 10 wameendelea kuenguliwa baada ya rufani zao kukataliwa na jumla ya rufaa, Rufaa 158 Tume ilikubaliana na maamuzi ya Wasimamizi wa Uchaguzi.

Rufaa tano (5) za Udiwani hazikukidhi hadhi ya kuwa rufaa kutokana na kutokidhi masharti ya kisheria. Rufaa hizo tano (5) ni zile ambazo zilikuwa ni kuomba kuwaondoa Wagombea wanaoendelea na Kampeni za Uchaguzi.
2.13.Viti Maalumu

Ibara ya 66 (1) (a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kifungu 86A cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, pamoja na kifungu cha 86A cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292 vinatoa utaratibu namna ya Tume itakavyoshughulikia upatikanaji wa Wabunge na Madiwani Wanawake Viti Maalum.

Vyama vyote vya Siasa vinatakiwa kuwasilisha orodha ya Wanawake wanaopendekezwa kuwa Wabunge na Madiwani wa Viti Maalum ndani ya siku therathini (30) kabla ya siku ya Uchaguzi. Tarehe ya mwisho kwa Vyama vya Siasa kuwasilisha majina na Fomu za Viti Maalum ilikuwa ni tarehe 25 Septemba 2015.
Jumla ya Vyama vya siasa tisa (9) tu ndivyo vimewasilisha fomu na majina ya wagombea wa Viti Maalum mpaka ilipofika siku ya mwisho, yaani tarehe 25 Septemba, 2015. Vyama hivyo ni CCM, CUF, UPDP, UMD, TLP, DP, NLD na ACT-Wazalendo. Vyama vingine mpaka sasa havijawasilisha orodha kama Sheria inavyosema.

2.14.Kampeni na Maadili ya Uchaguzi
Itakumbukwa kuwa Vyama vya Siasa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Serikali walisaini Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madawani tarehe 27 Julai 2015.

Lengo la maadili hayo ni kuhakikisha kunakuwepo na uwanja sawa katika kuwezesha vyama kushiriki katika Uchaguzi kwa Amani na Utulivu ili kuwezesha vyama kutoa sera zao na wananchi kuweza kuwasikiliza na kufanya maamuzi baada ya kuwasikiliza Wagombea.

Hadi sasa Tume ngazi ya Taifa imeshapokea na kutolea maamuzi malalamiko mawili (2) kutoka Vyama vya Siasa kulalamikia uvunjwaji wa maadili hayo.
Changamoto ambayo Tume imekuwa ikikumbana nayo ni Vyama vya Siasa na Wagombea kutotii maadili kama yalivyokubaliwa na baadhi ya vyama na Wagombea kutowasilisha malalamiko yao katika kamati za maadili na badala yake kukimbilia katika vyombo vya habari.

2.15. Vifaa vya Uchaguzi
Manunuzi ya vifaa vya Uchaguzi yameshafanyika vifaa hivi ni pamoja na Karatasi za Kura, fomu mbali mbali, lakiri, mihuri ya Vituo, wino maalum vyeti vya Ushindi wa Bunge na Diwani, mfano wa karatasi za kura Daftari na Orodha ya Wapiga Kura na mabango ya elimu ya mpiga kura.
Tume imeshapokea vifaa vyote vya uchaguzi na kuvisambaza katika Halmashauri mbalimbali.

Vifaa ambavyo havijasambazwa ni pamoja na Karatasi za Kura, Wino maalum, Karatasi za Matokeo ya Kura na Muhuri wa Kituo.vifaa hivi vitasambazwa hivi karibu.
2.16.Uteuzi na Mafunzo kwa Watendaji wa Ngazi Mbalimbali
Tume ya Taifa ya Uchaguzi ndiyo yenye mamlaka ya kisheria kuteua na kutoa mafunzo kwa watendaji wa Uchaguzi. Watendaji hao wanajumuisha Waratibu wa Uchaguzi (RECs), Wasimamizi wa Uchaguzi (ROs), Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi (AROs) na Wasimamizi wa Vituo (Presiding officer) na Makalani waongozaji (Direction Clerks).
Jumla ya watendaji 30 ngazi ya Mkoa, 972 Ngazi ya jimbo na 7914 ngazi ya Kata wameteuliwa na kupatiwa mafunzo.

2.17.Watazamaji wa Uchaguzi.
Tume kupitia wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ilitoa mwaliko kwa mashirika na Jumuiya za kimataifa na kikanda zinazotaka kuja kutazama Uchaguzi kuwasilisha maombi yao Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Kwa Upande wa Watazamaji wa ndani Tume kupitia vyombo vya habari ilizitaka Taasisi, Mashirika na Asasi za kiraia za ndani zinazotaka kuwa watazamaji wa Uchaguzi kuwasilisha maombi yao kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Jumla ya Taasisi kumi na mbili (12) za kimataifa na Sabini na Tano (75) za ndani zimewasilisha maombi yao kuwa watazamaji wa Uchaguzi
2.18.Upigaji, uhesabuji kura na utangazaji wa matokeo
Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeshatangaza kuwa tarehe 25/10/2015 kuwa ni siku ya kupiga kura, na vituo vitafunguliwa kuanzia saa 1:00 asubuhi na kufungwa saa 10:00 jioni.

Kwa mujibu wa Ibara ya 5 (1) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kifungu cha 63 (1) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura 343, Mtu anayeruhusiwa kupiga kura ni:
  1. Raia yeyote wa Tanzania aliyetimiza umri wa miaka 18 na ameandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na awe na kadi ya kupigia kura, iliyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania.
  2. Mkazi wa kawaida wa eneo analotaka kupiga kura
  3. Jina lake limeorodheshwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na katika orodha inayobandikwa katika kituo cha kupigia
    kura.
Aidha, Kwa mujibu wa Kifungu cha 61 (3) (e) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi sura ya 343 taratibu zifuatazo zitafuatwa katika Upigaji kura
  1. Vituo vitakuwa na wakala wa Vyama vya Siasa wakati wote wa zoezi la upigaji kura. Kituo kisipokuwa na wakala, Msimamizi wa Kituo hazuiwi kuendelea na zoezi la kupiga kura.
  2. Kila Mpiga Kura atapiga kura katika kituo alichojiandikishia atatakiwa kuonyesha kadi yake kama uthibitisho kuwa yeye ni Mpiga Kura.
  3. Kwa Mpiga kura asiyeona na asiyejua kusoma na kuandika ataruhusiwa kusaidiwa na mtu mwingine tofauti na Msimamizi wa Kituo, Msimamizi msaidizi wa kituo na wakala wa chama.
  4. Msimamizi wa kituo atahakiki jina la Mpiga Kura huyo kama lipo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura la kituo hicho na kisha atamruhusu kupiga kura.
13
Baada ya zoezi la upigaji kura kukamilika na Kituo kufungwa, Kituo cha upigaji kura hugeuka na kuwa Kituo cha kuhesabia kura, ambapo kura zote za Urais, Ubunge na Udiwani huhesabiwa na kubandikwa matokeo yake nje ya Kituo.

Zoezi la ubandikaji wa Matokeo likikamilika Wasimamizi wa kituo na Mawakala husindikiza Karatasi za matokeo na masanduku ya kura hadi katika Kata husika ambapo ujumlishaji wa matokeo ya Kata nzima ya Diwani, Msimamizi Msaidizi wa ngazi ya Kata humtangaza mshindi wa ngazi ya Udiwani na kumkabidhi Cheti cha ushindi.
Msimamizi Msaidizi na Mawakala wa Vyama vya Siasa husindikiza karatasi za matokeo ya Kura za Rais na Mbunge na masanduku ya kura yote hadi Jimbo husika ambapo ujumlishaji wa kura za Rais na Ubunge ngazi ya Jimbo hufanyika na ushughulikiaji wa kura zenye migogoro, baada ya zoezi la ujumlishaji kukamilika Msimamizi wa Uchaguzi humtangaza mshindi wa kiti cha ubunge na kumkabidhi Cheti cha ushindi,

Baada ya zoezi la ujumlishaji wa matokeo ngazi ya Jimbo, matokeo ya Urais hutumwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambao hufanya ujumlishaji wa matokeo ya Urais wa majimbo yote na kumtangaza mshindi wa kiti ya Urais
Ikumbukwe kuwa kwa mujibu wa Kifungu cha 80 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Sura ya 343 na kifungu cha 81 cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi ndio yenye mamlaka kisheria kujumlisha na kutangaza matokeo ya Uchaguzi wa Rais

Wasimamizi wa Uchaguzi wa Majimbo husika ndio wenye mamlaka kisheria kujumlisha na kutangaza matokeo ya Uchaguzi wa Wabunge.
Na Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi ndio wenye mamlaka ya kujumlisha na kutangaza matokeo ya Udiwani.

2.19.Mfumo wa Menejimenti ya Matokeo (Result Management System)
Mfumo huu ni mfumo ulioandaliwa na Tume kwa ajili ya kuondoa makosa mbalimbali ya kibinadamu yanayoweza kutokea kwa bahati mbaya katika zoezi la ujumlishaji wa matokeo umekamilika.
Kasoro/ makosa hayo ni kama ujumlishaji wa matokeo ya kituo kimoja mara mbili, kukosea uandikaji wa 7 badala ya 1, usahihi wa ujumlishaji n.k. mfumo huu sio mgeni kwani ulitumika katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 na 2010. Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 mfumo huu ulisanifiwa upya na kutumika, hata hivyo, kasoro chache zilionyeshwa.
Kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 Tume imeboresha mfumo na kuondoa mapungufu katika maeneo yote yaliyokuwa na changamoto mwaka 2010.
Tume imeandaa mfumo mbadala wa (Spreadsheet Excel RMS) ambao utatumika iwapo kutakuwa na changamoto katika kutumia mfumo uliondaliwa.

Jana tarehe 11.10.2015 Tume iliwaalika Wataalam wa TEHAMA kutoka vyama vyote vya Siasa na kupitishwa katika Mfumo huo.

2.20.Utumaji wa Matokeo kutoka katika Majimbo ya Uchaguzi
Utumaji wa matokeo ulikuwa na changamoto nyingi katika Uchaguzi wa mwaka 2010. Kati ya Majimbo 239 ni majimbo 150 tu yaliweza kutuma matokeo kwa mfumo uliokuwa umeandaliwa ambao ni kupitia mtandao wa simu za mikononi, matokeo yaliyobaki yalitumwa kwa nukushi (Fax).
Kwa sasa Tume inafanya maandalizi ya kutumia mkongo wa mawasiliano wa Taifa, kutuma matokeo yote badala ya kutumia mtandao wa simu za mikononi. Hii itasaidia upatikanaji wa matokeo mapema kama inavyokusudiwa. Hata hivyo njia mbadala ya kutuma matokeo kwa nukushi (Fax) imeandaliwa na Halmashauri zote zimepatiwa vifaa vitakavyowezesha utumaji wa matokeo kwa haraka kufanyika.

Aidha, Tume imekubaliana na TAMISEMI kuhusu kutumia Mkongo wa mawasiliano wa TAMISEMI ili kuweza kusaidia utumaji wa taarifa za matokeo kutoka katika Halmashauri hadi Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
2.21.Elimu ya Mpiga Kura

Tume imepewa mamlaka kisheria ya kutoa Elimu ya Mpiga Kura kuratibu na kusimamia watu au Taasisi zinazotoa Elimu ya Mpiga Kura.
Jumla ya Asasi za kiraia 451 ziliomba kutoa Elimu ya Mpiga kura, kati ya hizo ni Asasi 447 zilikidhi vigezo na hivyo kupewa kibali cha kutoa Elimu ya Mpiga Kura. Asasi hizi zilisaini Maadili ya Utoaji wa elimu ya Mpiga kura na kukubali kutumia mwongozo wa Elimu ya Mpiga kura.

Kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2015, Tume imeandaa zana mbalimbali za Elimu ya Mpiga kura ikiwemo mabango na vijitabu mbalimbali kama vile mpango mkakati wa Utoaji wa Elimu ya Mpiga Kura, Mwongozo wa Elimu ya Mpiga kura, Maswali yaulizwayo mara kwa mara, mwongozo kwa Mpiga kura, Uchaguzi huru ni kielelezo cha Demokrasia, Wagombea na Vyama vya Siasa katika Uchaguzi Mkuu 2015. Malengo yake ni Kuelimisha na kuhamasisha wananchi ili washiriki kikamilifu katika mchakato wa Uchaguzi kwa kuongeza idadi ya Wapiga Kura na kupunguza idadi ya Kura zinazoharibika.

Pamoja na vijitabu hivi Tume imekuwa ikishiriki katika vipindi mbalimbali vya radio na Tv ili kuweza kutoa taarifa, ufafanuzi na elimu kwa Umma kuhusu mambo mbali mbali yahusuyo mchakato wa Uchaguzi.
Pamoja na mwamko mkubwa unaoonyeshwa na Asasi za Kiraia katika kutoa Elimu ya Mpiga Kura kuhusu Uchaguzi Mkuu Tume imebaini kuwepo kwa changamoto kadhaa katika utekelezaji wa zoezi hilo kama ifuatavyo:
  1. Baadhi ya Asasi kutopata fedha kutoka kwa wafadhili na hivyo kushindwa kutoa elimu ya Mpiga Kura.
  2. Baadhi ya Asasi kutoa elimu zenye Itikadi za kisiasa
  3. Kutokuwepo kwa chombo cha kuratibu na kusimamia utoaji wa Elimu ya Uraia, kunakosababisha Elimu ya Uraia kutotolewa kwa utaratibu mzuri na kutotofautishwa na Elimu ya Mpiga Kura.
  4. Baadhi ya Asasi za Kiraia zinazopewa fedha za kutoa Elimu ya Mpiga Kura na wafadhili kutotoa Elimu ya Mpiga Kura kama ilivyokusudiwa.

2.22.Changamoto za mandalizi ya Uchaguzi Mkuu
Tume imekuwa ikikabiliana na changamoto mbalimbali kuelekea Uchaguzi Mkuu wa tarehe 25 Oktoba 2015.
  1. Changamoto ya kwanza ni Vifo vya Wagombea wa Ubunge na Udiwani ambavyo vimetokeo.Tume imepokea taarifa za vifo vya Wagombea wa Ubunge Majimbo ya Lushoto (CHADEMA), Ulanga Mashariki (CCM), na Wagombea wanne wa Viti vya Udiwani. Mchakato wa Uchaguzi wa Ubunge Majimbo ya Lushoto, Ulanga Mashariki na udiwani katika Kata hizo utakuwa kama ifuatavyo:
    •   Uteuzi 12 Octoba 2015
    •   Kampeni 13 Octoba 2015-18 Novemba 2015
    •   Siku ya Kupiga Kura 22 Novemba 2015
      Ikumbukwe kuwa tarehe 25-26/10/2015 hakutaruhusiwa Kampeni za aina yoyote kwakuwa ni siku ya Uchaguzi na Utangazaji wa matokeo
      Aidha, Tume imepokea taarifa ya Kifo cha Mgombea Ubunge jimbo la Arusha Mjini kwa Tiketi ya ACT Maendeleo. Tume imetoa taarifa rasmi ya kusimamisha shughuli za uchaguzi wa Ubunge katika jimbo hilo na itatoa taarifa kuhusu tarehe ya Uteuzi, Kampeni na Uchaguzi katika jimbo hilo.
  2. Changamoto ya pili ni Vyama vya Siasa kuendelea kutoa taarifa za upotoshaji kwa Wapiga Kura na pia kutoa tuhuma zisizo na uthibitisho kuhusu Tume, ambayo imepelekea Tume kutumia
muda mwingi kutoa ufafanuzi kuhusu tuhuma zinazotolewa na Vyama hivyo.

3. HITIMISHO
Uchaguzi ni kazi kubwa na muhimu inayohusisha wadau wengi hasa vyama vya siasa na mafanikio yake yanategemea zaidi kujituma na ushirikiano mzuri kati ya Tume na vyama vyama vya siasa. Tume kwa upande wake imejipanga kuhakikisha kuwepo kwa ufanisi mkubwa katika kuendesha na kusimamia Uchaguzi Mkuu wa 2015 kwa kuzingatia sheria zilizopo. Tume inatarajia vyama vya siasa kushiriki kikamilifu katika kuwahamasisha na kuwaelimisha wananchi kwa ujumla kuhusu mchakato wa uchaguzi kwa lengo la kuwa na Uchaguzi ulio huru, haki na uwazi zaidi ili kulinda amani, kuleta mshikamano katika taifa na kukuza Demokrasia na utawala Bora nchini.

“KURA YAKO MUSTAKABALI WAKO
KAPIGE KURA ILI KUMCHAGUA KIONGOZI UNAYEMTAKA
AHSANTENI KWA KUNISHIRIKISHA
MWISHO
















Hakuna maoni:

Chapisha Maoni