USIUZE KADI YAKO

USIUZE KADI YAKO

Focusradiotz

Jumamosi, 10 Oktoba 2015

UKWELI KUHUSU VIFAA KAMA BVR VILIVYOKAMATWA KATIKA KIWANDA CHA MMI STEEL MILLS

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
KUHUSU TUHUMA ZA KUKAMATWA KWA BVR MACHINE
Tume ya Taifa ya uchaguzi inapenda kutoa taarifa kwa vyombo vya Habari na Umma kwa ujumla kuwa Tume ilipokea taarifa toka kwa mmoja wa viongozi wa  CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA)  kuwa kuna uandikishaji wa wapiga kura unaofanyika katika eneo la viwanda Mikocheni.

Baada ya Tume kupata taarifa hiyo, kwa kushirikiana na Viongozi wa CHADEMA ilichukuwa jukumu la kufuatilia  suala hilo ili kubaini ukweli na kuchukuwa hatua stahiki kama kungekuwa na zoezi hilo ambalo ni kinyume cha  za sheria za Uchaguzi.

Hata hivyo, baada  ya Uongozi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na uongozi wa  CHADEMA kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kufuatilia suala hilo katika kiwanda cha MM Intergrated Steel Mills   ilibainika kuwa vifaa hivyo vilikuwa vinatumika kwa minajili ya kuandaa kanzi data (data base) ya wafanyakazi wa kiwanda hicho ili kuwa na taarifa sahihi za wafanyakazi wao.

Vifaa vilivyopatikana katika kiwanda hicho, ambavyo CHADEMA walishuku kuwa vinatumika kuandikisha Wapiga kura ni ‘Dell Laptop’, ‘Toshiba Laptop’, ‘Web Camera’, ‘CPU’, na ‘Finger Print scanner’.

Aidha, kutokana na kutokuwa na uhakika wa moja kwa moja kuwa nini kilikuwa kinafanyika katika vifaa hivyo, Mtaalamu wa TEHAMA toka Tume ya Taifa ya uchaguzi alishauri kuwa Vifaa hivyo vichukuliwe na Polisi na kukabidhiwa kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Uongozi wa CHADEMA ili wataalamu wa TEHAMA toka Tume ya Taifa ya Uchaguzi washirikiane na wataalamu wa TEHAMA toka CHADEMA wajiridhishe pasipo shaka   iwapo ni kweli au siyo kweli kuwa vifaa hivyo vinafanya kazi ya kuandikisha Wapiga kura.

Oktoba 9, 2015, Wataalamu wa TEHAMA wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, CHADEMA na wale wa MM Intergrated steel mills walikutana pamoja katika Ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi ili kukagua vifaa hivyo ili kujiridhisha kuwa vifaa hivyo havikuwa vinatumika kwa ajili ya kuandikisha wapiga kura.

MATOKEO YA UCHUNGUZI
Wataalamu wa TEHAMA wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na wale  wa CHADEMA walivichunguza vifaa hivyo na kubaini pasipo shaka kuwa vifaa hivyo havikuwa vinatumika kuandikisha Wapiga kura kama   taarifa iliyotolewa na CHADEMA bali vifaa hivyo vilikuwa vinatumika kuandikisha na kuhifadhi kumbukumbu za wafanyakazi kwa ajili ya matumizi ya kiwanda.

Aidha, baadhi ya vifaa kama kifaa cha kuchukulia alama za vidole cha MM Intergrated steel mills (MMI) hawakatazwi kuwa nacho kwani wanakitumia kwa ajili ya kazi zao na si kwa ajili ya uandishaji wapiga kura kama CHADEMA walivyowatuhumu. Uchunguzi uliofanyika umebaini kuwa ziko ofisi nyingi za serikali ambazo zina vifaa kama hicho na wanavitumika kwa matumizi husika. Mfano ni TRA na Uwanja wa ndege.

Uchunguzi huo pia ulibaini kuwa, vifaa hivyo vina kanzidata (SQL server 2008R2) ambayo ina taarifa ya Wafanyakazi wa MM Intergrated steel mills na siyo vinginevyo na ina sehemu mbili ambazo ni Motisun Group na Test kama ambavyo zilibainika katika uchunguzi huo.

 UTOJIA WA TAARIFA SAHIHI
Baada ya kukamilika kwa uchunguzi uliofanywa na wataalamu wa TEHAMA wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na wale wa CHADEMA,Tume ya Taifa ya Uchaguzi inavisihi vyama vya siasa kuepuka na kuacha kutoa taarifa za upotoshaji kwa kigezo cha kutaka kuonekana vipo makini  katika ufuatiliaji na utoaji taarifa.
Kitendo cha kusema na kujiaminisha kuwa unachosema ni sahihi ni kitendo cha kuonesha kutoaminika pale inapodhihirika ulichosema siyo sahihi ni uwongo na upotoshaji mkubwa.

Aidha CHADEMA ni vyema wakawaelimisha  mashabiki, wafuasi na wananchama wao kufuata taratibu za mawasiliano na kuepuka kusambaza taarifa za propaganda katika mitandao ya Kijamii ili kuepusha mhemko miongozi mwa watu hasa wakati huu ambapo joto la kisiasa nchini liko juu.

Vile vile kwa kuwa uchunguzi wa kina umeshafanyika na kubaini kuwa kanzidata ya MM integrated steel mills haina uhusiano wowote na ile ya Tume ya Taifa ya uchaguzi,Tume inakitaka  CHADEMA kuhakikisha kuwa usambazaji wa picha za BVR kits ambazo zilitumika kuandikisha Wapiga Kura  zilizosambazwa na maafisa wao waliokuwa katika zoezi hili katika mitandao ya kijamii zinasitishwa mara moja ili kuepuka kuendelea kuupotosha umma kuhusiana na tuhuma  zisizokuwa na ukweli

Tume inapenda kusisitiza kuwa taarifa zote zinazotolewa kwa umma lazima zithibitishwe pasipo shaka ili kuondoa mkanganyiko katika jamii na kuepusha wananchi kuchukua hatua ambazo zinaweza kuleta uvunjifu wa Amani.

Kwa kuwa Uchunguzi wa kina umeshafanyika na kubaini kuwa vifaa vilivyokuwa vinatumika havina uhusiano wowote na BVR kit za Tume ya Taifa ya uchaguzi,Tume inalitaka gazeti la NIPASHE ambalo limekuwa linaripoti kuwa kuna BVR bandia (fake) zimekamatwa waombe radhi kwa kuupotoshwa umma kwa kuandika taarifa sahihi kuhusiana na kile kilichoonekana katika kiwanda hicho badala ya taarifa walizoandika kupitia gazeti la Nipashe toleo na 0578632 la tarehe 10,oktoba 2015.

Kwa kumalizia, Tume ya Taifa ya Uchaguzi inapenda kusisitiza kuwa Amani na mustakabali wa   nchi hii uko katika matendo na maamuzi tutakayoyafanya leo. Hivyo ni muhimu kuhakikisha kuwa kila jambo linalijitokeza linapewa tahadhari na umakini wa kutosha ili tusiharibu Amani na Mshikamano tulionao hivi sasa.
Imetolewa na

Kailima R. Kombwey
MKURUGENZI WA UCHAGUZI
Hakuna maoni:

Chapisha Maoni